Utawala wa kijeshi wa Burkina faso wavunja vyama vya siasa

Utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso umevivunja vyama vyote vya siasa nchini humo pamoja na kufuta sheria zinazosimamia vyama hivyo, hii ikiwa ni kulingana na amri iliyodhinishwa na serikali siku ya Alhamisi.

Waziri wa Mamlaka za Maeneo Emile Zerbo amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya mamlaka kugundua kwamba vyama hivyo vinakiuka miongozo ya kuanzishwa kwao, kusababisha migawanyiko miongoni mwa wananchi na kudhoofisha muundo wa kijamii.

Shughuli za vyama vya siasa kwa muda mrefu zimezuiwa chini ya utawala wa kijeshi na amri hiyo inataka mali za vyama hivyo kuhamishiwa serikalini, limearifu shirika la habari la serikali.

Wanaharakati wanasema hatua kama hizo zimelenga uhuru wa raia na upinzani tangu mamlaka ya kijeshi ilipochukua mamlaka katika mapinduzi ya 2022.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii