Makamu rais wa zamani wa Kenya adai jaribio la kumuua katika shambulio la Kanisa

Mwanachama maarufu wa upinzani nchini Kenya Rigathi Gachagua amedai kulikuwa na jaribio la kumuua wakati wa ibada ya siku ya Jumapili kanisani.

Gachagua, alitimuliwa kwenye wadhifa wake kama makamu wa rais mwaka wa 2024, alidai kundi la maafisa wa polisi wasio na nidhamu walishambulia kanisa huko Othaya katika kaunti ya kati ya Nyeri, kwa kutumia risasi na gesi ya machozi.

Bila kutoa ushahidi wowote, alimshutumu mshirika wake wa zamani, rais William Ruto, kwa kuagiza shambulio hilo. Ruto hajajibu, lakini Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen amelaani vurugu hizo, akiziita hazikubaliki.

Polisi imetangaza kufunguliwa kwa uchunguzi na kuthibitisha kwamba hakuna majeraha yaliyoripotiwa.

Kulingana na ripoti za polisi, bomu la machozi linadaiwa kutupwa ndani ya Kanisa la Anglikana la St. Peter saa 11:00 asubuhi kwa saa za huko, na kukatiza ibada.

Magari kadhaa yanaripotiwa kuharibiwa katika uwanja wa kanisa, polisi imeongeza, ambayo imetoa wito wa kujitokeza kwa mashahidi.

Gachagua, mfanyabiashara tajiri kutoka eneo la Mlima Kenya katikati mwa Kenya na sasa mkosoaji mkubwa wa rais, amesema alipelekwa salama hadi nyumbani kwake na timu yake ya usalama.

Alichapisha picha za tukio hilo kwenye mtadao wa kijamii wa X na baadaye akafanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alikanusha madai ya wanablogu wanaounga mkono serikali kwamba shambulio hilo lilikuwa limeandaliwa na wahusika ili kuchafua idara za usalama.

"Tunaweza kupata wapi mabomu ya machozi?... Tunaweza kupata wapi bunduki za kiita za AK-47?" aliuliza kiongozi wa chama cha Demokrasia kwa Wananchi.

Alisema kwamba mkuu wa polisi alimuahidi washambuliaji hao watafikishwa mahakamani.

"Ghasia, popote zinapotokea, na hasa mahali pa ibada, hazikubaliki," Waziri wa Mambo ya Ndani alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X.

"Polisi lazima wachukue hatua bila woga au upendeleo dhidi ya  wale walioamuru na kutekeleza kitendo hiki, bila kujali hadhi yao ya kijamii au chama cha kisiasa."

Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, hukumu ya Gachagua kwenye Bunge la Seneti inamzuia kushikilia tena wadhifa wowote serikalini.

Alikana mashtaka kumi na moja dhidi yake lakini alipatikana na hatia katika mashtaka matano, ikiwa ni pamoja na kuchochea chuki za kikabila na kukiuka kiapo chake cha urais.

Hata hivyo, mwanasiasa huyu, anayejulikana zaidi kama Riggy G, anasisitiza kwamba atagombea katika uchaguzi wa urais mwaka ujao, kwani amekata rufaa na Mahakama Kuu bado haijatoa uamuzi wa kuondolewa kwake.

Ruto na Gachagua walichaguliwa kwa tiketi ya pamoja mwaka wa 2022. Muungano huu uliwezesha Ruto kushinda uchaguzi kwa kuhamasisha uungwaji mkono wa wapiga kura katika Mlima Kenya, makao makuu ya watu wa Kikuyu, ambao wanaunda kambi kubwa zaidi ya wapiga kura nchini Kenya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii