Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja zinashirikiana
kutekeleza mfumo wa anwani za makazi nchini kwenye mikoa yote 31 ya
Tanzania Bara na Zanzibar ili iweze kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka
huu kwa lengo la kufanikisha zoezi la sensa ya watu inayotarajiwa kuanza
mwezi Agosti mwaka huu ambapo uzinduzi wa operesheni ya anwani za
makazi na kikao kazi kwa ajili hiyo kimefanyika leo kwenye ukumbi wa
Sheikh Idriss Abdul Wakil, Zanzibar
Mgeni Rasmi wa kikao kazi na
uzinduzi wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Makamu wa Pili wa Rais,
Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa tuna viongozi katika
kila ngazi, kila mmoja akifanya kazi yake vizuri hakuna mzanzibari
atakosa taarifa kuhusu anwani za makazi na sensa ya watu na tumeona
wataalam wetu wa ndani wametengeneza mfumo wa NaPA ambao unatupatia
anwani za makazi ambapo tungetumia wataalam wa nje, Serikali ingetumia
fedha nyingi sana
Ameongeza kuwa Serikali itagawa shilingi
bilioni 28 kwenye mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajiili
ya utekelezaji wa anwani za makazi na ugawaji huo wa fedha hizo
utazingatia ukubwa wa maeneo na mahitaji halisi ya eneo husika
“Fedha
hizi zitakuja kwenye mikoa yenu, zikatumike kwa makusudi yaliyokusudiwa
na tutazifuatilia kwa karibu, naamini viongozi ni wasikivu na mtatoa
ushirikiano ipasavyo ili tufanikiwe utekelezaji wa jambo hili la anwani
za makazi kwa kuwa hakutakuwa na muhali kwenye jambo hili na mmefanikiwa
kwenye mazoezi makubwa na hili naamini nidhamu ya matumizi ya fedha
itafanyika na tukitoka hapa tukawaelimishe wananchi wetu kuhusu jambo
hili na tujumuishe kwenye ajenda zetu zote” amesisitiza Mhe. Abdullah
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar (Sera, Uratibu na
Baraza la Wawakilishi), Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed wakati
akimkaribisha mgeni rasmi amesema kuwa masuala haya yanahitaji
ushirikiano wa pamoja na ndio maana wote tuko hapa na baada ya kikao
hiki kila mmoja achukue jukumu lake la kuhakikisha anwani za makazi na
sensa ya watu inakamilika ipasavyo
“Ni lazima wananchi wajue
kibao hiki kipo hapa kwa manufaa gani hivyo ni muhimu kujenga uelewa kwa
wananchi ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kupatikana”, amesisitiza
Mhe. Mohammed.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa mazoezi haya mawili ya utekelezaji
wa mfumo wa anwani za makazi na sensa ya watu ni mazoezi mawili tofauti
ila yanayotegemeana ambapo operesheni hii imelenga kuliongezea nguvu
zoezi la sensa ya watu kwa sababu ya maagizo mliyotupatia kuwa zoezi la
anwani za makazi linatakiwa kuisha mwezi wa tano na la sensa litaanza
mwezi wa Nane mwaka huu
Waziri Nape ameongeza kuwa zoezi la
anwani za makazi ni safari ya kuelekea Tanzania ya kidijitali kwa kuwa
bila anwani za makazi Tanzania ya kidijitali haiwezakani kwa kuwa tayari
dunia imeshaenda kidijitali, sisi ni sehemu ya dunia na kama tunataka
kwenda kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ni lazima tutekeleze mfumo wa
anwani za makazi na Zanzibar ya kidijitali inawezekana
Amefafanua
kuwa mfumo huu wa anwani za makazi ni mkataba baina ya CCM na wananchi
kuwa ifikapo mwaka 2025 tuwe na awani za makazi na ni uamuzi mzuri kuwa
jambo hili litekelezwe kwa miezi mitano badala ya miaka 5
“Zoezi
la sensa haliwezi kutekelezwa vizuri bila anwani za makazi, hivyo
tumeona ni vema mfumo wa anwani za makazi utekelezwe kwanza ili
kufanikisha utekelezji wa sensa ya watu na makazi,” amesema Waziri Nape
Ameongeza
kuwa utekelezaji wa mfumo huu wa anwani za makazi ungetekelezwa na
wakandarasi ungetumia zaidi ya shilingi bilioni 700 ila Serikali
itatumia shilingi bilioni 28 tu kwa kuwa mfumo huu wa operesheni ya
anwani za makazi ni mali ya wananchi na utatekelezwa na wananchi wenyewe
mpaka kwenye ngazi ya Serikali ya Mitaa/Shehia na utasimaimwa na
watendaji wa Serikali ya Mitaa/Shehia wenyewe
Naye Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Amour Bakari amesema kuwa Wizara hizi zenye dhamana ya
Mawasiliano ikiwemo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari ya Tanzania Bara zinawajibika kuhakikisha kuwa anwani za makazi
zinatekelezwa kwa kuwa anwani za makazi zinawezesha mwananchi kupata,
kupokea na kufikisha huduma au bidhaa hivyo tunapaswa kuwa na anwani za
makazi kwa kuwa anwani ni nyenzo muhimu ya mawasiliano nchini na hadi
sasa jumla ya shehia 30 kati ya shehia 338 za Zanzibar zina anwani za
makazi ambayo ni sawa na asilimia 7 tu.
Katika kikao kazi hicho,
wataalam wa kutoka Wizara na taasisi za SMZ waliwasilisha taarifa kuhusu
hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka
2022; Sensa ya Majengo; na taarifa ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za
makazi ambapo kwa upande wa Tanzania Bara, mtaalam wa TEHAMA, Fredrick
Apina kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
aliwasilisha kwa viongozi hao namna mfumo wa NaPA unavyofanya kazi
ikiwemo ukusanyaji wa taarifa na matumizi yake kwa mwananchi katika
shughuli za kiuchumi na kijamii ambapo mfumo huu unamwezesha mwananchi
kupata anwani za maeneo mbali mbali na huduma zinazotolewa mahali alipo
au yaliyo jirani nae
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Makamisaa wa Sensa; Makatibu Tawala wa Mikoa; Wakuu wa
Wilaya; Makatibu Tawala wa Wilaya; Wakurugenzi wa Miji; Mabaraza ya
Manispaa na Halamashauri za Wilaya; Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za
Serikali uliofanyika kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil,
Zanzibar.