Waasi wanaoiunga mkono na Urusi nchini Ukraine wamevituhumu vikosi vya serikali kwamba vimeshambulia kwa makombora kijiji kimoja hii leo. Tuhuma hizo zimetolewa wakati vyombo vya habari vya Urusi kwa upande mwingine vikiripoti kwamba wanajeshi na magari ya kivita ya Urusi yanaelekea kwenye kambi zao kinyume na khofu inayooneshwa na nchi za Magharibi juu ya uwezekano wa Urusi kuivamia Ukraine. Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax kwa siku ya pili mfululizo waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine wamesema wameshambuliwa kwa mizinga na makombora na wanajeshi wa serikali ya Ukraine. Jana Alhamisi serikali ya Urusi ilisema ina wasiwasi mkubwa na mashambulio hayo yaliyozuka nchini Ukraine na inafuatilia kwa karibu. Marekani hata hivyo imesema Urusi inatafuta sababu ya kuhalalisha vita. Rais Joe Biden jana alisema Urusi inaandaa mazingira ya kuhalalisha uwezekano wa kufanya shambulio dhidi ya Ukraine, ambayo lengo lake la kutaka siku moja kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO limeikasirisha Urusi.