Algeria yatinga hatua ya mtoano ya AFCON nchini Morocco

Algeria imekuwa nchi ya tatu baada ya Misri na Nigeria kutinga hatua ya mtoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika - AFCON 2025. Iliifunga Burkina Faso bao moja kwa sifuri mjini Rabat kupitia mkwaju wa penalti wa Riyad Mahrez.

Ambapo Mahrez sasa ana jumla ya mabao matatu kwenye mashindano hayo huku Algeria ambao ni mabingwa wa Afrika mwaka wa 1990 na 2019 wana pointi sita baada ya mechi mbili za Kundi E na hawajafungwa bao.

 Katika Kundi F mabingwa watetezi Ivory Coast walishindwa kujiunga na nchi hizo tatu baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na Cameroon katika mechi ya kusisimua iliyopigwa mjini Marrakesh.

Aidha bao la Ivory Coast lilitiwa kimiani na winga wa Manchester United Amad Diallo. Timu hizo mbili zina pointi nne kila mmoja huku Msumbiji ikiwa na tatu.

Kwingineko Msumbiji ilipata ushindi wao wa kwanza wa AFCON baada ya kusubiri kwa miaka 39 kwa kuifunga Gabon 3 - 2 katika mtanage uliopigwa kwenye mji wa kusini wa Agadir. 

Nayo Sudan ilirejea katika nafasi za kufuzu hatua ya 16 za mwisho kwa kuifunga Guinea ya Ikweta bao moja kwa sifuri mjini Casablanca.

Hata hivyo  Sudan wanashiriki mashindano ya AFCON nchini Morocco licha ya nchi hiyo kuharibiwa vibaya tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF Aprili 2023.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii