Ethiopia yaanza kuzalisha umeme katika bwawa la mto Nile

Bwawa lenye utata la Ethiopia kwenye mto wa Nile lilianza kuzalisha umeme kwa mara ya kwanza Jumapili, kulingana na runinga ya serikali.

Bwawa hilo lenye thamani ya $4.2bn (£3.8bn), lililoko magharibi mwa eneo la Benishangul-Gumuz, limekuwa chanzo cha mzozo kati ya Ethiopia, Misri na Sudan tangu ujenzi wake uanze mwaka wa 2011.

Sudan na Misri zinahofia mradi huo unaweza kupunguza sehemu yao ya maji ya Nile.

Ethiopia inasisitiza kuwa bwawa hilo ni muhimu kwa maendeleo yake.

Bwawa linaloitwa Grand Ethiopian Renaissance Dam (Gerd) ni mradi mkubwa zaidi wa umeme wa maji barani Afrika hadi sasa.

Gerd inatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 za umeme, na hivyo kuongeza pato la taifa la umeme maradufu itakapokamilika kikamilifu.

Kwa sasa limekamilika kwa asilimia 83.9, kituo cha habari cha ETV kinachomilikiwa na serikali kilisema Jumapili.


Serikali ya Ethiopia inasisitiza kuwa itabadilisha uchumi wa taifa, ambao umeharibiwa vibaya na ukame na vita, utakapoanza kufanya kazi kikamilifu.

Katika hafla ya ufunguzi siku ya Jumapili, Bw Abiy alizuru kituo cha kuzalisha umeme katika bwawa hilo na kubofya vitufe kadhaa ambavyo vilianzisha utayarishaji wa uzalishaji, kulingana na maafisa.

"Hizi ni habari njema kwa bara letu na nchi za chini ambazo tunatamani kufanya kazi pamoja," Bw Abiy aliandika kwenye Twitter.

Lakini ujenzi wa bwawa hilo umesababisha mfarakano kati ya Misri na Sudan.

Ethiopia imekuwa ikielekeza maji ya Nile kujaza hifadhi kubwa nyuma ya bwawa hilo.

Misri, ambayo iko chini ya mto na inategemea karibu kabisa na Mto Nile kwa umwagiliaji wake na maji ya kunywa, ina wasiwasi hii itaathiri viwango vya maji yanayoingia nchini.

Kwa hiyo inataka uhakikisho wa kiasi fulani cha maji yanayoingia Misri.

Lakini Ethiopia inasitasita kuhusishwa na takwimu fulani ya kiasi cha maji ya kutoa kwani kipaumbele chake ni kuhakikisha kuna maji ya kutosha kuendesha mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme barani Afrika.


Sudan pia ina wasiwasi kuhusu jinsi bwawa hilo litaathiri viwango vyake vya maji.

Mwaka jana, Sudan ilishikwa na mshangao wakati Ethiopia ilipoamua kufunga vituo vitatu kati ya vinne vya kuelekeza maji.

Hii ilisababisha viwango vya chini vya maji kwenda chini ya mkondo ambayo ilitatiza vituo vya kusukuma maji vya Sudan kwa ajili ya umwagiliaji na usambazaji wa maji katika manispaa.

Nchi zote mbili zimekuwa zikigombea makubaliano na Ethiopia juu ya kujaza na uendeshaji wa bwawa hilo, lakini mazungumzo yameshindwa kufanikiwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii