Urusi na China zimetoa wito kwa Marekani kumuachilia kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro pamoja na mke wake Cilia Flores kufuatia kukamatwa kwao katika operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Urusi, China na Venezuela zimetoa mwito kwa Marekani kumuachilia kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro pamoja na mke wake Cilia Flores.
Mabalozi wa nchi hizo tatu katika Umoja wa Mataifa wamekosoa kile walichokiita kitendo cha uchokozi wa Marekani na ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Katika kikao maalum cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika New York jana Jumatatu, Urusi na China zimelaani vikali hatua ya Marekani kumkamata kiongozi huyo wa Venezuela mwishoni mwa wiki.
Urusi imeilezea hatua ya Marekani kama "ishara ya kurejea katika enzi ya kukosekana kwa sheria na utawala wa Marekani kwa nguvu, machafuko na uhalifu," ikisema hali kama hiyo inaendelea kuzikumba nchi kadhaa duniani.
China kwa upande wake imesema hakuna nchi yoyote inayoweza kujifanya kuwa polisi wa dunia wala kujipa mamlaka ya kuwa hakimu wa kimataifa.
Nchi nyingine zilizokosoa hatua ya Washington ni Cuba, Iran, Colombia pamoja na Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime