Rais wa Marekani Donald Trump ametoa onyo kali kwa wabunge wa chama chake cha Republican huku akisema kuwa kushindwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Novemba 2026 kutawapa Democrats fursa ya kumng’oa madarakani kupitia mashtaka ya kikatiba.
Akizungumza hayo Jumanne katika mkutano wa faragha wa wabunge wa Republican mjini Washington Trump amesema kuwa ushindi katika uchaguzi huo ni muhimu kwa mustakabali wa urais wake na utekelezaji wa ajenda za chama hicho.
“Lazima mshinde uchaguzi wa katikati ya muhula. Msiposhinda, watatafuta sababu yoyote ya kuniondoa madarakani. Nitang’olewa,” alisema Trump kwa msisitizo.
Aidha katika hotuba yake iliyodumu kwa dakika 84 Trump amewataka wabunge hao kuweka kando migawanyiko ya ndani na kujikita katika kuuza sera za Republican kuhusu masuala nyeti yakiwemo jinsia huduma za afya na uadilifu wa uchaguzi.
Amesisitiza kuwa ujumbe huo ulengwe hasa kwa wapiga kura wanaokerwa na kupanda kwa gharama za maisha, akitambua pia changamoto ya kihistoria ambapo chama cha rais aliyeko madarakani hupoteza viti vingi katika uchaguzi wa katikati ya muhula.
Huku akikabiliwa na shinikizo la umma kuzingatia zaidi masuala ya ndani kama mfumuko wa bei Trump amedai kuwa alirithi tatizo hilo kutoka kwa utawala wa Democratic aidha amewahimiza Republicans kujivunia ongezeko la thamani ya masoko ya hisa kama ushahidi wa mafanikio ya kiuchumi.
Hivyo basi katika hotuba hiyo Trump pia amejivunia kile alichokitaja kuwa operesheni ya kijeshi iliyofanikiwa dhidi ya kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro hatua ambayo imezua mjadala kuhusu mwelekeo wa sera zake za kigeni.
Kwa mujibu wa Trump ambaye aliwahi kufunguliwa mashtaka ya kikatiba mara mbili katika muhula wake wa kwanza kati ya mwaka 2017 na 2021 na kuachiwa huru na Baraza la Seneti, sasa anakabiliwa na tishio jipya. Baadhi ya wabunge wa Democratic wanaripotiwa kuanza kuandaa hati za mashtaka mapya, wakimtuhumu kwa matumizi mabaya ya madaraka katika muhula wake wa pili.
Hata hivyo uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2026 unaonekana kuwa mtihani mkubwa kwa utawala wa Trump na hatima ya kisiasa ya chama cha Republican katika Bunge la Marekani.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime