Mamlaka ya Rwanda imetangaza hitimisho la kwanza la uchunguzi wake kuhusu kutoweka kwa mshairi Innocent Bahati, ambaye familia yake haijasikia habari zake kwa mwaka mmoja. Katika gazeti linalounga mkono serikali, Idara ya Upelelezi ya Rwanda ilimshutumu mshairi huyo mnamo Jumatano Februari 16 kwa kuwa na uhusiano na vuguvugu la waasi.
Akihojiwa na Gazeti la mtandaoni la Taarifa, msemaji huyo wa Idara ya Upelelezi ya Rwanda (RIB) anadai kuwa na ushahidi unaoonyesha kuwa Innocent Bahati aliondoka kwenda Uganda ambako alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na makundi yanayopinga utawala wa Rwanda, kwa mujibu wa istilahi iliyotumiwa kwenye makala. Pia anatuhumiwa kushirikiana na vuguvugu linalopinga serikali ya Rwanda lenye makao yake makuu nchini Ubelgiji na Marekani.
Hakuna maelezo zaidi kutoka kwa mamlaka kwa sasa, wala taarifa rasmi. Uchunguzi haujafungwa na Innocent Bahati bado hajapatikana, kwani Idara ya upelelezi inabaini kwamba mtuhumiwa huyo aliweza kuondoka Uganda na kuelekea nchi nyingine.
Kauli hizi zinakuja siku kumi baada ya barua ya wazi kutoka kwa shirika la Pen International, iliyotumwa kwa Rais Paul Kagame, na kutiwa saini na waandishi vitabu mia moja akiwemo Margaret Atwood na Salman Rushdie. Walieleza kuwa walikuwa na sababu ya kuamini kuwa kutoweka kwa Innocent Bahati kulihusishwa na uandishi wake na matatizo ya kijamii aliyoibua katika mashairi yake kwenye mtandao wa YouTube.
Rwanda inashutumiwa mara kwa mara kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza. Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilikadiria katika ripoti ya mwezi Machi 2021 kwamba kutoweka kwa mwandishi huyo kunapaswa kuchukuliwa kuwa ni jambo la kutiliwa shaka, na kubaiani kwamba kuna "visa vya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa wakosoaji wa serikali nchini Rwanda".