DRC kukabiliwa na janga la njaa.

Mzozo wa kibinadamu bado unaendelea kutatanisha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Umoja Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na mamlaka wanatangaza kwamba wanahitaji karibu dola bilioni 2 ili kukabiliana na mzozo wa chakula unaochochewa na umaskini, machafuko mashariki mwa nchi, magonjwa ya milipuko na utapiamlo.


Mpango huu wa kukabiliana na mzozo wa kibinadamu ulizinduliwa Alhamisi Februari 17 mjini Kinshasa, lakini kuna matumaini madogo ya kukusanya fedha zinazotakiwa.

Dola bilioni moja na milioni 880 ndizo  fedha zinazotafutwa na serikali na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu. Kiasi hiki kikubwa kinapaswa kuwezesha kusaidia karibu watu milioni 9 waliogawanywa katika makundi 5 yanayopewa kipaumbele yaliyoorodheshwa na Suzanna Tkalec, afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada ya kibinadamu nchini humo.

"Ni watu waliokimbia makazi yao, watu waliorejea kutoka ukimbizini, wakimbizi na jamii, watoto, watu walio katika hatari na waathirika wa ukatili wa kijinsia, wanawake wajawazito, na watu wanaoishi na ulemavu".

Vigezo vingine havijabadilika: huku watu milioni 27, au robo ya wakazi wake wakiishi katika hali hii, DRC ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi katika uhaba wa chakula duniani.

DRC pia ni nchi ambayo ina idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.

Umoja wa Mataifa umehesabu zaidi ya watu milioni 5 waliokimbia makazi yao. Hali inatisha, lakini wafadhili hawana uhakika kuwa wanaweza kukidhi mahitaji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii