Wananchi wa Dar es Salaam wameendelea kuonesha malalamiko yao kutokana na ukosefu wa maji safi katika maeneo mbalimbali ya jiji, hali ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maisha ya kila siku. Tatizo hili limeathiri matumizi ya nyumbani, shule, na biashara ndogo ndogo, huku familia nyingi zikikosa maji.
Wakazi wamesema wanashangazwa na kuendelea kupokea bili za maji kila mwezi, licha ya huduma hiyo kutowafikia.
Miongoni mwa maeneo yenye tatizo kubwa ni Tabata, Kisukulu, Kwa Mkua, Makoka Shule ya Msingi, Ubungo, Sinza, Mwenge Mpakani, pamoja na maeneo mengine yanayozunguka jiji.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, hivi karibuni alisisitiza kwamba huduma ya maji itatolewa kwa mgao na kwa usawa, kuhakikisha kila sehemu ya Dar es Salaam inapata huduma hii muhimu. Hata hivyo, baadhi ya wananchi bado hawajapata maji, jambo ambalo limeendelea kuwa changamoto katika mwezi wa pili mfululizo.
Wananchi wanaiomba Wizara ya Maji na mamlaka husika kuhakikisha usambazaji wa maji unakuwa wa haki, endelevu, na unafikiwa kwa wakati ili kuondoa usumbufu unaokumba familia na biashara ndogo ndogo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime