Umoja wa Mataifa kuzikutanisha pande hasimu nchini Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliambia shirika la Habari la Al Arabiya la Saudi Arabia kuhusu mkutano huo, ingawa hakufichua tarehe ya mazungumzo hayo.

Katika hatua hiyo maafisa wa Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kukutana mjini Geneva na pande zinazohasimiana nchini Sudan katika juhudi za kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mgogoro unaoendelea nchini humo.

Aidha Guterres amesema kuwa Umoja wa Mataifa umehakikishiwa kuwa njia za kuingia mji wa El-Fasher ambao bado umekatwa mawasiliano, zitafunguliwa hivi karibuni, huku RSF ikiendelea kudhibiti upatikanaji wa huduma za intaneti na setilaiti za Starlink.

Matumaini ya kupatikana kwa mwanga katika mazungumzo kuhusu vita vya Sudan yaliongezeka mwezi uliopita baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kueleza utayari wa kusaidia kuumaliza mzozo huo kufuatia ombi la mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman wakati wa ziara yake mjini Washington.

Hata hivyo Tangu mnamo Aprili mwaka 2023, jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF vimekuwa vikipigana na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya takriban watu milioni 12 kuyahama makaazi yao.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii