Nchini Ufaransa, muungano wa vyama vya kiraia kwa ajili ya Rwanda (CPCR) umewasilisha mahakamni malalamiko dhidi ya Benki ya Ufaransa, ukiishutumu kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda. Taarifa hiyo, iliyofichuliwa na Gazeti la Libération na Radio France, inatokana na mfululizo wa uhamisho wa fedha unaoshukiwa ambao unadaiwa uliwezesha kupewa silaha kwa vikosi vya mauaji ya kimbari.
Kati ya mwezi Mei na Agosti 1994, wakati mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda yalikuwa yamefikia kilele chake, uhamisho saba ulifanywa kutoka kwa akaunti ya Benki ya taifa ya Rwanda (BNR), iliyofunguliwa katika Benki ya Ufaransa. Jumla ya kiasi: faranga milioni 3.17, au takriban euro 486,000. Wakati huo, BNR ilikuwa ikisimamiwa na mamlaka ya mauaji ya kimbari.
Malalamiko hayo, yaliyowasilishwa Desemba 4 kwa jaji mkuu wa uchunguzi wa kitengo cha "uhalifu dhidi ya ubinadamu" huko Paris, yanatafuta kubaini kama Benki ya Ufaransa ilishindwa katika majukumu yake ya usimamizi, ikizingatiwa kwamba Umoja wa Mataifa uliweka vikwazo vya silaha Mei 17, 1994.
Kulingana na wataalamu kadhaa wa Umoja wa Mataifa waliotajwa katika malalamiko hayo, uhamisho huo unadaiwa kutumwa kwa kampuni ya Ufaransa Alcatel, inayoshukiwa kutoa vifaa vya mawasiliano, pamoja na balozi kadhaa za Rwanda.
Kulingana na Alain Gauthier, aliyewasilisha malalamiko hayo, lengo lilikuwa kununua vifaa vya kijeshi. "Unaponunua silaha, uhamisho huo haufanyiki moja kwa moja." "Pesa zilipitishwa kupitia balozi, namna ya kuficha jinsi pesa hizo zilivyotumwa," anaelezea mlalamikaji.
Ushuhuda unataja, haswa, ununuzi wa simu za setilaiti, ambazo zilizingatiwa kuwa za kimkakati na serikali ya mpito ya Rwanda wakati huo ili kudumisha mawasiliano yake.
Swali linabaki: Benki ya Ufaransa ilijua nini kuhusu mwisho wa uhamisho huu? Kwa nini haikuuzuia, haswa wakati wa marufuku ya silaha? Alain Gauthier anabainisha kwamba isingeweza kujua hali hiyo: "Mnamo Mei 14, Umoja wa Mataifa ulitangaza marufuku ya silaha. Kila mtu anajua."
Benki ya Ufaransa inakanusha kosa lolote. Inadai kuwa haikupata dalili yoyote ya uhamisho huo uliotajwa hapo juu, huku ikibainisha kuwa uchunguzi wake ulibaki "wazi," muda ukiwa "mfupi sana" tangu malalamiko hayo yalipowasilishwa. Hta hivyo benki hiyo inakumbusha kwamba sheria inaitaka kuharibu hati hizi baada ya miaka kumi.
Mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000 kati ya mwezi Aprili na Julai 1994, kulingana na Umoja wa Mataifa.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime