Michael Masi aondolewa kama mkurugenzi wa mbio za F1

Michael Masi ameondolewa kama mkurugenzi wa mbio za magari ya langalanga kama sehemu ya urekebishaji katika bodi ya FIA kufuatia mashindano ya Abu Dhabi Grand Prix ya mwaka jana.

Rais wa FIA Mohammed ben Sulayem alitangaza msururu wa mabadiliko kutokana na uchunguzi wa mwisho wenye utata wa michuano ya Dunia ya mwaka jana.

Masi alishindwa kutumia sheria kwa usahihi aliporuhusu gari la dharura kuingia barabarani katika mzunguko wa mwisho wa makala ya mwisho ya mbio za magari ya langalanga na hilo lilikuwa na athari ya moja kwa moja kwenye matokeo ya mbio za ubingwa.

Wanaume wawili sasa watapishana katika jukumu hilo, huku usaidizi wa ziada utatolewa kwa maafisa.

Wakurugenzi wapya wa mbio hizo watakuwa Eduardo Freitas, ambaye hapo awali alikuwa na jukumu hilo katika Mashindano ya Dunia ya Endurance, na Niels Wittich, ambaye alikuwa na jukumu hilo hilo katika Mashindano ya Magari ya Kutalii ya DTM ya Ujerumani.

Freitas na Wittich watasaidiwa na mkongwe wa F1 Herbie Blash, ambaye alikuwa naibu mkurugenzi wa mbio chini ya mkurugenzi wa zamani wa FIA F1 Charlie Whiting.

Masi alichukua jukumu la mkurugenzi wa mbio wakati Whiting alipofariki dunia usiku wa kuamkia msimu wa F1 wa 2019.

Masi "atapewa nafasi mpya ndani ya FIA," Ben Sulayem alisema.

Mjini Abu Dhabi, Masi alipata shinikizo kutoka kwa timu zote mbili za Mercedes na Red Bull kufanya maamuzi ya kuwapendelea.

Mzozo mkubwa baada ya mbio hizo uliibuka kutokana na ukweli kwamba alionekana kufuata mapendekezo ya Red Bull, kwa faida ya dereva wao Max Verstappen juu ya Lewis Hamilton wa Mercedes.

Baada ya Masi kushindwa kutumia sheria kwa njia mbili - juu ya usimamizi wa njia za magari na muda wa kuanza tena - Verstappen alitumia matairi yake mapya kumpita Hamilton na kushinda taji lake la kwanza la dunia.

Kumbuka kuwa kuweko kwa gari barabarani wakati wa mashindani kuna masharti kwa madereva wa mbio za langa langa kwanza hawaruhusiwi kwenda kwa kasi na pili hawaruhusiwi kupita magari mengine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii