Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, jana ameongoza
Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, waumini wa Kiislam na wananchi
mbali mbali katika Hauli ya kumkumbuka na kumuombea Dua maalum Marehemu
Maalim Seif Sharif Hamad.
Dua
hiyo maalum imefanyika huko Masjid Jibirili Mkunazini jijini Zanzibar
na ilisimamiwa na Sheikh Abdurahman Alhabshy kwa khitma na nyiradi
mbali mbali za kumuombea maghfira Marehemu Maalim Seif.
Waliohudhuria
katika dua hiyo ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Zitto
Zuberi Kabwe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Ndugu Juma Duni Haji,
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wake Zanzibar, Salim Abdalla Bimani, Katibu
Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume,
Wanachama na Viongozi waandamizi wa ACT-Wazalendo, masheikh, waumini na
wananchi mbali mbali visiwani hapa.
Marehemu Maalim Seif
alifariki dunia tarehe 17 Februari mwaka jana huko Hospitali ya Taifa
Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu na kuzikwa siku ya pili yake
kijijini kwao Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo sasa ametimiza
mwaka moja tokea kufariki kwake.
Marehemu Maalim hadi anafariki
alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT- Wazalendo na pia Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, wadhifa ambao aliutumikia kuanzia tarehe
8 Disemba 2020 hadi tarehe 17 Februari 2021 alipofariki Dunia.
Mapema
wiki iliyopita Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Othman Masoud Othman
aliungana na viongozi mbali mbali wa ACT-Wazalendo pamoja na wakaazi wa
Pemba kulizuru Kaburi la Marehemu Maalim Seif huko Mtambwe pamoja na
kumuombea dua.
Hafla ya dua ilifanyika pia jana Kijijini kwa
Marehemu Maalim Seif, Nyali Mtambwe alikozikwa ambapo viongozi na
wananchi mbali mbali wa kisiwani Pemba walihudhuria.
Marehemu
Maalim Seif ambaye alikuwa mwanasiasa mkongwe, alitumikia nyadhifa
mbali mbali za kisiasa na serikali ikiwa ni pamoja na nyadhifa za Waziri
Kiongozi na Waziri wa Elimu kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar wadhifa ambao aliushikilia katika vipindi vya awamu
mbili tofati, baada ya maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye ACT-Wazalendo.
Marehemu
Maalim Seif pia atakumbukwa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Afrika na kwingineko duniani kutokana na michango na ushawishi
wake katika mageuzi ya siasa , sera, fikra na falsafa mtambuka kupitia
nyanja mbali mbali za maisha ya jamii, uchumi, upinzani, maendeleo na
maridhiano, sambamba na siasa za demokrasia ya kiliberali ulimwenguni.