Michuano ya kandanda kwa mataifa ya Afrika AFCON 2025 imeanza usiku wa kuamkia leo na katika mechi ya ufunguzi wenyeji Morocco waliibamiza timu ya taifa ya visiwa vya Commoro mabao 2-0.
Maelfu ya mashabiki walijitokeza kwa wingi katika uwanja wa Moulay Abdellah mjini Rabat kushuhudia ufunguzi rasmi wa michuano ya 35 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) huku Sherehe hizo zikihudhuriwa na Mwanamfalme Moulay Hassan wa Morocco, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Gianni Infantino pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Patrice Motsepe.
Hafla ya ufunguzi ilipambwa na burudani ya muziki pamoja na ngoma za kitamaduni, zilizowavutia mashabiki waliofurika uwanjani na waliokuwa wakifuatilia kupitia vyombo vya habari mbalimbali.
Baada ya sherehe hizo wenyeji Morocco waliingia dimbani na kuanza michuano hiyo kwa kishindo baada ya kuwashinda Comoro kwa mabao mawili bila majibu ambapo mabao hayo yalifungwa na Brahim Díaz na Ayoub El Kaabi, matokeo yaliyoiweka Morocco kileleni mwa msimamo wa kundi A huku Comoro wakibaki mkiani.
Hata hivyo Michuano ya hatua ya makundi inaendelea leo kwa michezo mitatu, ukiwemo ule unaosubiriwa kwa hamu kati ya Misri na Zimbabwe. Aidha, wawakilishi wa Afrika Mashariki, timu za Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, zinatarajiwa kushuka dimbani kesho Jumanne katika mechi zao za kwanza za mashindano hayo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime