Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Kamishna Mkuu
wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Salum Yussuf Ali, ili kupisha uchunguzi
wa kina wa upotevu wa fedha za makusanyo ya mapato zilizopotea.
Rais
Dkt. Mwinyi amefikia maamuzi hayo leo wakati akiwa katika Ofisi za Bodi
ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini Zanzibar ambapo alipata fursa ya
kuzungumza na uongozi wa Bodi ya Mapato, Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya
Mapato pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi
Zanzibar (ZAECA), mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi za
Mamlaka hiyo.
Wakati huo huo, taarifa maalum iliyotolewa kwa
vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said ilieleza utenguzi wa kiongozi huyo
alioufanya Rais Dkt. Mwinyi Februari 17, 2022.