WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali imepokea kauli ya wakazi wa Ngorongoro kwamba wako tayari
kupokea maelekezo ya Serikali na kushirikiana pamoja katika kuulinda
utalii na uhifadhi wa eneo hilo.
“Kwa kauli yenu kwamba mko
tayari kushirikiana na Serikali kuendeleza uhifadhi na kukuza utalii,
sisi tumeipokea na tutaitekeleza ahadi yenu”
Mheshimiwa Majaliwa
ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Februari 17, 2022) wakati
akizungumza na viongozi na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kwenye kikao
cha ndani kilichofanyika makao makuu ya zamani ya NCAA, wilayani
Ngorongoro, mkoani Arusha.
Amesema, kama ambavyo Serikali imetoa
nafasi ya kusikiliza maoni ya wananchi wa tarafa hiyo, nao hawana budi
kuipa nafasi Serikali kuendelea na mpango wa maboresho wa maeneo ambayo
yanatakiwa kufanyiwa uhakiki ili ije na mpango bora wa kuliendeleza eneo
hilo.
Amesema atapitia changamoto alizokabidhiwa na Diwani wa
Naiseko, Bw. James Moringe na akawataka wakazi hao waendelee kuiamini
Serikali yao kwa sababu ina nia njema na wananchi wake.
“Endeleeni
kuiamini Serikali yenu kwani ina njema na nyie. Tunahitaji kuona
shughuli za ufugaji zikiendelea na utalii ukiendelea. Na kwa maana hiyo,
mnakubaliana na Watanzania wanaotaka kuona utalii ukiendelea. Na kwa
maana hiyo tufuate misingi ya uhifadhi.”
“Na mnapotoka hapa, kila
mmoja wetu akatafakari kuhusu changamoto ya kuongezeka kwa mifugo na
idadi ya watu. Muwe watulivu wakati Serikali ikifanyia kazi maoni yenu.
Tutapokea pia maoni ya taasisi na asasi za kiraia, nazo pia tutazifanyia
kazi,” amesisitiza.
Amesema Serikali itaratibu maoni
yanayotolewa na pande zote. “Tunapofanya hilo, mahali pote tunaangalia
maslahi ya Taifa. Wana-Ngorongoro endeleeni kuiamini Serikali yenu,
endeleeni kumuamini Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu na endeleeni
kuamini miongozo inayotolewa kwani ina tija kwenu.”
“Wakati wote
Mheshimiwa Rais amesema anawapenda Watanzania wake na ni kweli
anatupenda sana. Yeye ndiye mtumishi nambari moja na sisi ni wasaidizi
wake na ni lazima tufuate philosophy yake ambayo anataka kuona
Watanzania wanasikilizwa na wanashauriwa.”
Waziri Mkuu amesema
muendelezo wa vikao anavyofanya katika wilaya ya Ngorongoro ni
utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya
kuwataka viongozi wakutane na wakazi hao na kuwasikiliza maoni yao.
Mkutano
huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi,
TAMISEMI, Naibu Waziri wa Ardhi, Makatibu Wakuu wa wizara za Maji na
TAMISEMI na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa dini.
Wadau
walioshiriki kikao ni Mbunge wa Ngorongoro, Malaigwanan, Wenyeviti wa
vijiji na Vitongoji, Baraza la Wafugaji la Ngorongoro, viongozi.