Serikali
kupitia Wizara ya Afya imepokea vifaa vya Tehama na machapisho vyenye
thamani zaidi ya Mil. 105 kwa ajili ya kusambazwa kwenye vituo vya Afya
ili kuboresha huduma za ufuatiliaji na udhibiti magonjwa ya milipuko
nchini Tanzania.
Vifaa
hivyo vimetolewa Februari 17,2022 na Shirika lisilo la kiserikali la
“Management and Development for Health –(MDH)” kupitia ufadhili wa
rasilimali fedha na ushauri wa kitaalam kutoka kituo cha kudhibiti
magonjwa cha Marekani-CDC, ofisi ya Tanzania.
Akiongea
wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Oparesheni wa MDH Dkt. Nzovu
Ulenga amesema wamekabidhi vifaa hivyo ni pamoja na Kompyuta mpakato
(laptops), vishwikwambi (tablets), projectors, Printers na vifaa
mbalimbali vya stationary kwa ajili ya kazi za machapisho ya ripoti za
kisayansi na maabara.
“MDH
kupitia ufadhili huu, inapenda kutoa shukrani za dhati kwa wafadhili
wetu CDC, Wizara ya Afya na TAMISEMI pamoja na wadau wetu wengine katika
kubuni na kutekeleza mikakati yote ya Kisera na Kitaalam katika
kufuatilia na kuthibiti magonjwa ya mlipuko yanayoathiri mfumo wa njia
ya
upumuaji.”amesema Dkt. Ulenga
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi msaidizi Epidemiolojia na udhibiti wa
magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Rogath Kishimba baada ya kupokea
amesema vifaa hivyo vitakwenda kusaidia kutoa taarifa kwa vituo rasmi
vya kukusanya taarifa za Magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
“Natoa
Shukran kwa shirika la kudhibiti na kuzuia Magonjwa pamoja na shirika
la MDH kwa kutoa vifaa hivi vitakavyo kwenda kurahisisha utendaji kazi
na kuwahudumia wagonjwa kwa haraka.” amesema Dkt. Kishimba
Vifaa
hivyo pia vitakwenda kusaidia Katika kupambana na magonjwa ya mlipuko,
katika maeneo matatu ambayo ni uwezo wa kutambua / kugundua visababishi
vya magonjwa, pili ni kutoa taarifa kwa haraka na ubora na tatu ni
kuchukua hatua sahihi za kupambana na ugonjwa husika kwa kufuata taraibu
za Nchi na za kimataifa.