Makamu wa rais wa Kenya ajitetea kuhusu ukosefu wa ngombe DR Congo

Naibu rais wa Kenya amejitetea baada ya kuibua hasira katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na matamshi yake ya awali yaliyoashiria kuwa hakuna ngombe nchini humo.

William Ruto alisema wakati wa mkutano wa kisiasa kwamba kuna soko kubwa la mazao ya maziwa ya Kenya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sababu "watu hawa ambao ni waimbaji tu…hawana ngombe yoyote."

Hata hivyo kauli hiyo haikuwaendea vyema watu wengi wa Congo, ambao baadhi yao walimshutumu Bw Ruto kwa kukosa heshima.

Mnamo Jumatano jioni, Bw Ruto alisema anajutia “kutoelewana ambako kunaweza kuwa kumetokea kwasababu ya hotuba yangu“.

Alisema hotuba yake haikuwa rasmi na haikukusudiwi kudharau lakini ilikuwa ikisisitiza ‘’ukubwa wa fursa” nchini DR Congo.

Balozi wa Kenya nchini DR Congo alisema maoni hayo yamesababisha “maoni hasi miongoni mwa jumuiya ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla”.

“Ubalozi wa Kenya ungependa kusisitiza kwamba serikali na watu wana uhusiano wa kina na wa heshima; uhusiano wa kihistoria na serikali na watu wa [DRC],” George Masafu alisema katika taarifa yake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii