Chama apewa kazi maalumu

Ushindi  wa mabao 3-1  umewafurahisha sana viongozi wa Simba na sasa katika kujipanga kuhakikisha wanaendeleza kasi hiyo ugenini dhidi ya USGN ya Niger na ile ya RS Berkane ya Morocco umempa kazi maalumu Clatous Chama.

Simba ilianza vyema mechi zake za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na Jumapili watavaana na USGN mjini Niamey, Niger.

Katika kuhakikisha mambo yanaendelea kuwa laini, benchi la ufundi la Simba limeamua kumtumia Chama katika mechi hizo za ugenini kwa kumjumuisha katika kikosi kinachoondoka jijini Dar es Salaam leo.

Kikosi cha Simba kinaondoka na wachezaji 24 akiwemo Chama ambaye licha ya kutokuwa sehemu ya mechi hizo kutokana na kwamba alishaichezea RS Berkane katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini ana kazi maalumu ya kuisaidia timu hiyo.

Mmoja wa viongozi wa Simba amelifichulia Mwanaspoti kwamba, wanaondoka na Chama kwa vile ni mzoefu kwenye mechi za kimataifa na kuwahi kucheza Morocco, wakiwa na nia ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini.

“Tumeamua kusafiri na Chama ambaye tunatambua kabisa kuwa hatakuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza katika mchezo huo, ila kuna sababu za kiufundi ambazo ndizo zimetufanya kusafiri naye,” alisema mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Mulamu Nghambi.

Licha ya wenyeji wa Simba (USGN), kufungwa mabao 5-3 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya RS Berkane haijawapoteza maboya viongozi wa wana Msimbazi kuwachukulia poa.

Mulamu alisema wameweka mambo sawa ili kuhakikisha timu inaenda kupata ushindi ugenini.

Alifafanua kuwa walituma watu kwenda Niger kufanya uchunguzi na tayari wamekamilisha suala la usafiri, sehemu ya kufikia na chakula.

“Ili timu ifanye vizuri lazima viongozi tuweke mazingira sawa kama usafiri, sehemu ya timu kufikia na chakula ambavyo vipo tayari. Kilichobaki ni kazi uwanjani,” alisema Mulamu.

“Baada ya mchezo huo tutaweka kambi Niger inaweza kuwa siku nne au tano kujiandaa na RS Berkane.”

Mulamu alisema katika msafara wao unaoondoka leo saa 7 mchana, mbali na Chama pia una wachezaji wengine wote isipokuwa Chris Mugalu, Denis Kibu na Hassan Dilunga walio majeruhi.

Mulamu alisisitiza wanatambua mchezo utakuwa mgumu, licha ya wenyeji wao USGN kupoteza kwa mabao 5-3 dhidi ya RS Berkane.

“Benchi la ufundi linafanya kazi yake ya kuwafuatilia wapinzani, viongozi tunafanya kazi yetu ya kuweka mazingira ya wachezaji kuwa vizuri na tumefanya hivyo,” alisema

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii