Droo ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Kandanda Duniani, FIFA, litakalofanyika mwakani huko Marekani, Canada na Mexico itafanyika leo katika Kituo cha Sanaa cha Kennedy huko mjini Washington.
Kombe hilo la dunia litashuhudia jumla ya nchi 48 kushiriki hiyo ikiwa ni mara ya kwanza idadi kubwa kama hiyo ya nchi zimeshirikishwa mashindano hayo ya dunia.
Miongoni mwa timu zitakazoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo ya duniani ni Cape Verde, Curacao, Jordan na Uzbekistan.
Rais wa Marekani Donald Trump, mwenzake wa Mexico Claudi Sheinbaum pamoja na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney watahudhuria droo hiyo pamoja na Rais wa FIFA Gianni Infantino.
Timu 11 bora duniani kulingana na orodha ya FIFA zimefuzu mashindano hayo. Argentina inayoongozwa na nahodha wao Lionel Messi, itakuwa inatafuta kulitetea taji hilo walililoshinda huko Qatar katika mashindano yaliyopita.