Kilimo Chatangazwa Kama Kituo Kipya cha Mafanikio kwa Vijana

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Said Mtanda ametoa wito mahsusi kwa vijana kujikita katika sekta ya kilimo na kusema kuwa wakati umefika kwa vijana kuitumia ardhi kama njia ya kujijenga kiuchumi kupitia mbinu za kilimo cha kisasa, teknolojia mpya na fursa za mikopo.

Amezungumza  hayo  leo Desemba 3 mwaka huu wakati akifungua warsha ya TADB na waandishi wa habari mkoani humo huku akieleza kuwa kilimo ni sekta yenye uwezo mkubwa wa kuongeza ajira, kukuza uzalishaji na kuchochea maendeleo kwa kasi mpya inayolingana na dira ya taifa.

Mtanda ameendelea kusisitiza kuwa kilimo si kazi ya kukimbia bali ni injini ya mafanikio ambayo vijana wanapaswa kuimiliki sasa ambapo amewahamasisha vijana waone kilimo kama eneo la fursa, uvumbuzi na uthubutu na ndicho kituo sahihi cha kujenga mustakabali imara wa maisha yao na taifa kwa ujumla.

Kwa upande Meneja wa Kanda ya Ziwa kutoka TADB Frank Nyabundege ametumia jukwaa hilo kufafanua dhamira ya Benki ya Kilimo katika kuendeleza uchumi wa viwanda kupitia uwezeshaji wa wakulima huku  akieleza kuwa TADB imejikita katika kutoa mikopo nafuu, kusaidia miradi ya thamani ya mazao, na kuimarisha mnyororo wa uzalishaji ili kuongeza tija ya kilimo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hata hivyo Nyabundege ametaja kwa msisitizo kuwa safari ya TADB Kanda ya Ziwa imejaa ushindi unaoonekana kwa macho, kuanzia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hadi miradi mipya ya vijana na vikundi vya wanawake inayochipua kwa kasi hivyo  dhamira ya benki si tu kutoa fedha, bali kuchochea mabadiliko ya fikra na kuwawezesha wananchi kuona kilimo kama biashara kamili kwa namna ya kipekee.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii