Bobi Wine "maisha yangu yako hatarini "

Mgombea urais wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine sasa anasema maisha yake yako hatarini na ameamua kuvaa koti la kuzuia risasi.

Hivi Karibuni, Bobi Wine na timu yake wamepambana na vikosi vya usalama na kusababisha matumizi ya risasi, mabomu ya machozi na kukamatwa kwa wafuasi.

Bobi Wine anavishutumu vikosi vya usalama kwa kuingilia kampeni yake kwa kuziba barabara na kuwakamata wafuasi wake huku vyombo vya usalama vikisisitiza kuwa Bobi Wine hafuati miongozo na kwamba wafuasi wake wamewashambulia kwa kutumia mawe. Sasa Bobi Wine ameamua kuanza kuvaa koti la kuzuia risasi.

"Unajua hatari tunayokabiliana nayo kutoka kwa vyombo vya usalama, kwa sababu hiyo nimeamua kuvaa koti la kuzuia risasi. Wenzangu wengi wamekuwa na wasiwasi na tumepata taarifa kwamba ninaweza kulengwa. Sijisikii salama kwa sababu ya koti hili lakini tunajaribu kufanya tuwezavyo kuzuia hatari lakini kwa ujumla tunajua Mungu ndiye mwenye nguvu Zaidi"

Vikosi vya usalama kwa upande mwingine vinamuonya yeye na wafuasi wake kuhusu kukiuka miongozo ya kampeni. Abas Byakagaba ni mkuu wa Polisi.

"Tuna wajibu wa kutekeleza sheria husika ili kuhakikisha utulivu wa umma ambao ni sharti la uchaguzi wa amani. Vitendo vya uchochezi, propaganda zenye madhara, matamshi ya chuki, kutangaza ukaidi, maandamano yasiyoidhinishwa ya kampeni, kuwashambulia wana usalama na uhalifu havitakubaliwa"

Uchaguzi unatarajiwa kufanyika tarehe 15 mwezi ujao na tume ya uchaguzi ambayo sasa inashughulikia matayarisho ya mwisho ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya kuwatambua wapiga kura imeliambia bunge kuwa inahitaji kwa haraka zaidi shilingi bilioni mia nne sitini na tisa nukta tano za Uganda.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii