Waziri wa Ulinzi wa Nigeria, Mohammed Badaru Abubakar, amejiuzulu wadhifa wake kutokana na sababu za kiafya, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais Bola Ahmed Tinubu.
Kujiuzulu kwa Abubakar, mwenye umri wa miaka 63, kunakuja wakati ambapo Nigeria inapitia kipindi kigumu cha kiusalama, huku serikali ikikabiliwa na mashinikizo makubwa kutokana na ongezeko la matukio ya utekaji nyara katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Wiki iliyopita, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa iliripoti kuwa watu 402 – wengi wao wakiwa wanafunzi wametekwa nyara tangu katikati ya mwezi Novemba.
Katika hatua ya kujaza nafasi hiyo, Rais Tinubu amemteua Jenerali mstaafu Christopher Musa, mwenye umri wa miaka 58. Jenerali Musa aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Majeshi ya Nigeria kuanzia Juni 2023 hadi Oktoba 2025 na amejulikana kwa utaalam wake katika mikakati ya kijeshi, hususan operesheni dhidi ya makundi ya kijihadi kaskazini-mashariki mwa nchi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime