Jeshi la DRC na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda, wamerushiana maneno kila mmoja akimtuhumu mwingine kukiuka makubaliano ya usitishaji mapigano, siku moja kabla ya viongozi wa Kinshasa na Kigali kukutana mjini Washington kutia Saini mkataba wa amani baina ya nchi hizo mbili.
Hapo jana Jeshi la Congo liliwatuhumu waasi hao kushambulia kambi zake zilizoko kwenye maeneo ya Kaziba, Katogota na Lubarika, madai ambao Kundi la M23 linadai lilikuwa linajibu mashambulio ya jeshi la FARDC na washirika wake wake Wazalendo.
Marekani na Qatar zimekuwa zikiratibu mazungumzo yanayolenga kurejesha amani katika majimbo ya Kaskazini na Kusini mashariki mwa DRC ambapo mapigano yamewalazimisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao.
Licha ya madai kuwa Rwanda inawasaidia waasi hao, Kigali imeendelea kukana kuwaunga mkono waasi hao, ambao wanadai wanapigana kulinda jamii za Watutsi mashariki mwa Kongo.
Haya yanajiri wakati hapo kesho rais Donald Trump atakuwa mwenyeji wa rais Felix Tshisekedi na Paul Kagame, ambapo watatia Saini makubaliano yatakayoshuhudia kumalizika kwa mgogoro wa mashariki mwa Congo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime