Vigogo wa Afrika, Young Africans SC ya Tanzania na Pyramids FC ya Misri, ndiyo timu pekee ambazo hadi sasa hazijaruhusu goli katika mizunguko miwili ya hatua ya makundi ya CAF Champions League, zikionesha uimara mkubwa kwenye safu zao za ulinzi.
Ngome ya Yanga imekuwa imara kwa kiasi kikubwa ikiongozwa na kipa wao mahiri Djigui Diarra, ambaye amekuwa nguzo kwa kucheza dakika zote 180 (mechi mbili) bila kuruhusu goli.
Diarra ameonesha ubora, utulivu na uongozi wa hali ya juu langoni, na kuchochea mjadala mpana barani Afrika kutokana na kiwango chake cha kuvutia.
Kwa upande wa Pyramids FC, kipa Ahmed El-Shenawy ameonesha ubora langoni, akicheza jumla ya dakika 127 bila kuruhusu goli, El-Shenawy alianza katika mechi ya kwanza na kucheza dakika zote 90 mechi ya pili alianza lakini akatolewa dakika ya 37 kufuatia kuumia bila kufungwa.
Kwa mujibu wa takwimu za CAF katika mizunguko miwili ya awali, hakuna timu nyingine iliyofanikiwa kulinda lango lao bila kuruhusu goli zaidi ya Yanga na Pyramids, jambo linaloonesha ubora wa safu zao za ulinzi, nidhamu ya kiufundi, na ubora wa makipa wao.
Mashabiki wa Yanga nchini Tanzania na wa Pyramids nchini Misri wana kila sababu ya kujivunia timu zao, huku wakisubiri kwa hamu kuona kama takwimu hizo zitadumu kwenye mizunguko mingine inayofuata.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime
Imeandikwa na @mustaphakinkulah