Marekani imetupilia mbali ripoti za Urusi kuondoa wanajeshi wake mpakani mwa Ukraine na badala yake ikaituhumu Moscow kwa kupeleka wanajeshi zaidi. Afisa mmoja mwandamizi katika Ikulu ya White House amesema Urusi imeongeza wanajeshi karibu 7,000 waliowasili jana Jumatano na kuyaita madai ya Moscow kuwaondoa wanajeshi wake kuwa ya uongo. Mapema siku ya Jumatano, Marekani, Jumuiya ya kujihami NATO ziliungana na Ukraine kusema kwamba hakuna dalili ya kuondolewa wanajeshi wa Urusi. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg, alikutana na mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya hiyo jana Jumatano, akidai kuwa kitisho katika mpaka wa Ukraine bado hakijakwisha. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo kujadili mzozo huo katikati mwa wasiwasi unaozidi kuongezeka juu ya uwezekano wa Urusi kuivamia Ukraine.