Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen J. Nindi, amesema kuwa Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano na Burundi katika Sekta ya Kilimo ili kuhakikisha wananchi wa nchi zote mbili wananufaika kikamilifu.
Dkt. Nindi amekutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Mifugo wa Burundi, Bw. Emmanuel Niyungeko Novemba 17 mwaka huu wakati wa ziara ya ujumbe wa Tanzania yenye lengo la kupanua wigo na kuimarisha masoko ya nafaka kikanda.
Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa chakula kupitia Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo 2050 (Agricultural Master Plan AMP 2050)na Ajenda 10/30, ikiwemo upimaji wa afya ya udongo nchi nzima ili kubaini aina za udongo na kuainisha pembejeo sahihi kwa kila eneo.
Aidha, maeneo mengine ni uimarishaji wa kilimo cha umwagiliaji, ambapo miradi zaidi ya 750 inaendelea kutekelezwa; kuimarisha Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika kusimamia ubora wa nafaka zinazoingia na kutoka nchini; uboreshaji wa matumizi ya zana za kilimo kwa kununua matrekta makubwa 1,000 na matrekta ya mkono 1,000; sambamba na kuanzisha vituo vya pamoja vya zana za kilimo kwa kushirikiana na vyama vya ushirika.
Katika ziara hiyo, Dkt. Nindi aliambatana na Balozi John Ulanga, Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew M. Komba.
Balozi Ulanga alisema kuwa Tanzania na Burundi zina nafasi kubwa ya kushirikiana katika kuendeleza biashara ya mazao ya nafaka ili kuimarisha usalama wa chakula katika ukanda mzima.
Aidha, Dkt. Komba alibainisha kuwa nchi hizo mbili zinaweza kuanzisha mfumo madhubuti wa ushirikiano utakaowezesha kukabiliana na changamoto za upungufu wa chakula, ikizingatiwa tofauti za vipindi vya tabianchi na uzalishaji wa mazao kati ya Tanzania na Burundi.