Balozi Mussa ameshiriki maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Angola

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, ameungana na viongozi mbalimbali wa serikali, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini katika hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Angola, iliyofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 11 mwaka huu.

Hafla hiyo imelenga kutambua safari ya maendeleo ya Angola tangu ilipopata uhuru wake Novemba 11, 1975, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya Angola na Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Mussa aliipongeza Angola kwa mafanikio makubwa iliyopata kisiasa, kijamii na kiuchumi, katika kipindi cha nusu karne ya uhuru wake, ambapo alieleza kuwa uongozi thabiti wa viongozi wa nchi hiyo, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, umewezesha Taifa hilo kuimarisha hatua za kujiletea maendeleo endelevu.

Balozi Mussa amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) mwaka 1981, Tanzania na Angola zimeendelea kuimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara, nishati, elimu, afya, utalii, na ulinzi. Amebainisha kuwa juhudi zinaendelea kufanyika ili kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Amesema Tanzania inathamini uhusiano wa kindugu uliopo kati yake na Angola, na itaendelea kushirikiana kwa karibu na Angola katika kuimarisha diplomasia, biashara na ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.

Alikumbusha mchango wa waasisi wa Tanzania na Angola, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Dkt. António Agostinho Neto wa Angola, katika harakati za ukombozi wa Afrika, ambao umeleta urithi mkubwa wa mshikamano, umoja, na heshima miongoni mwa mataifa ya Bara la Afrika.

Naye Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Angola nchini Tanzania, Bibi Julcimara Joaquim, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake thabiti na endelevu, kwani umechangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha maendeleo ya taifa la Angola na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama mshirika mkuu katika nyanja za maendeleo na ushirikiano wa kikanda.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii