Wakulima zaidi ya 250 katika Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza wamepokea jozi 22 za vifaa vya kisasa vya umwagiliaji kwa vikundi vyao 11, kufuatia lengo la Serikali la kusaidia kuondokana na utegemezi wa kilimo cha mvua.
Vifaa hivyo vimetolewa na Wizara ya Kilimo kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Nchini (TFSRP) ambavyo ni pamoja na pampu za maji, mipira ya umwagiliaji na vinyunyizi vya kisasa(sprinkler) ili kuongeza uzalishaji katika mazao ya chakula, biashara na kuongeza kipato kwa wakulima.
Hafla ya makabidhiano imefanyika katika Bonde la Mto Dutwa, Kata ya Lubugu Wilayani Magu Novemba 11 mwaka huu ambapo Mhandisi Makubi Abel kutoka Wizara ya Kilimo amesema kuwa TFSRP imekuwa ikisaidia wakulima wadogo kutumia teknolojia na mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija na kuleta zaidi mageuzi katika Sekta ya Kilimo nchini.
“Kilimo cha umwagiliaji ni suluhisho muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa mvua. Tunataka kuona wakulima wanatumia teknolojia hizi kwa tija ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato,” amesema Mhandisi Makubi.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Magu, Bw. Alphonce Awaki amewataka wakulima kuhakikisha wanavitumia vifaa hivyo kwa uangalifu, kuvitunza ipasavyo na kushirikiana katika matumizi yake ili viweze kudumu na kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa mazao.
Aidha, wakulima waliopokea vifaa hivyo wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na washirika wa maendeleo kwa kuwapatia msaada huo, wakieleza kuwa utawasaidia kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza mavuno, na kuboresha kipato chao.