Rais wa Kenya William Ruto, amesema kuwa demokrasia ni mfumo bora wa utawala, ingawa si rahisi kila wakati. Ameeleza kuwa demokrasia ina changamoto zake, lakini ni muhimu kwa mataifa yote kuilinda na kuendeleza utamaduni wa kusikiliza maoni mbadala bila kutumia nguvu au vurugu.
Amesema kuwa baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki bado zinapitia mabadiliko ya kidemokrasia, akisema Kenya iko hatua za mbele katika demokrasia ikilinganishwa na majirani wake.
Kauli hiyo ameitoa Novemba 9 mwaka huu huko Doha nchini Qatar alipohudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu maendeleo ya kijamii, ambapo alipata nafasi ya kufanya mahojiano na kituo cha Habari Kimataifa cha Aljazeera.
Katika mahojiano hayo Rais Ruto ameepuka kuzungumzia moja kwa moja kuhusu hali ya demokrasia nchini Tanzania, akisema kila taifa lina namna yake ya kuendesha masuala ya kisiasa.
Rais Ruto amehimiza ushirikiano wa kikanda katika kulinda demokrasia akisema viongozi wanapaswa kuzingatia maoni ya Wananchi na kuepuka kutumia nguvu katika kushughulikia tofauti za kisiasa.