Mwinyi amezindua rasmi Baraza la 11 la Wawakilishi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezindua rasmi Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar na kutoa mwelekeo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Nane, akisisitiza dhamira ya Serikali kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa msingi wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza leo Novemba 10 mwaka huu katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya CCM 2025–2030, pamoja na ahadi za kampeni na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nane.

Amesema Serikali itaendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kuimarisha sekta za uzalishaji, uwekezaji, sekta binafsi, na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwa na lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7 hadi 10 kwa mwaka, kudhibiti mfumko wa bei chini ya asilimia 5, kuzalisha ajira mpya 350,000, na kuongeza kipato cha mwananchi hadi Dola 1,880 kufikia mwaka 2030.

Aidha Serikali itatekeleza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, bandari za abiria Mpigaduri, Kizimkazi, Shumba na Wete, pamoja na boti mbili za kisasa za mwendo kasi zitakazohudumia safari kati ya Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salaam.

Katika sekta ya afya Serikali itajenga hospitali nne za mikoa kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Saratani Binguni na kuboresha Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Katika elimu Serikali itajenga madarasa mapya 2,000, shule tatu za sekondari za wasichana kwa kila mkoa, chuo cha kisasa cha ualimu, na kuajiri walimu 7,691.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha utumishi wa umma kwa kuongeza mafunzo maslahi na nidhamu ya kazi huku taasisi za ZAECA na CAG zikiimarisha mifumo ya udhibiti wa rushwa na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Ameongeza kuwa Afisi ya Usalama wa Shughuli za Serikali (GSO) itaongoza usimamizi wa nidhamu serikalini.

Vilevile Serikali itajenga vituo viwili vya utamaduni Unguja na Pemba, kuendeleza michezo, na kukamilisha maandalizi ya AFCON 2027.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii