Bondia wa Kitanzania, Lupakisyo Mohamedi Shoti, ameandika historia mpya katika ngumi za kulipwa baada ya kumshinda Mromania Daniel “Magic Dan” Buciuc na kutwaa mkanda wa IBO International Middleweight nchini Romania.
Pigano hilo la raundi 10 lilifanyika Ijumaa usiku kwenye ukumbi wa Sala Polivalentă, jijini Bucharest, katika pambano kuu la onyesho la “Ultimate Boxing Game”.
Buciuc aliingia ulingoni akiwa na rekodi ya mapambano 15 ushindi na1 kipigo, na akapigana mbele ya mashabiki wa nyumbani, huku Shoti akiwa ndiye mgeni ugenini akiwa na rekodi ya ushindi 8 na kipigo 1 kabla ya pambano.
Pamoja na tofauti hiyo ya uzoefu na mazingira, Mtanzania huyo alionyesha uimara na nidhamu ya hali ya juu ulingoni na kuibuka mshindi kwa pointi za majaji, akinyakua mkanda huo muhimu wa kimataifa uliokuwa wazi.
Shoti, anayesimamiwa na Fayheroes Sports Promotion na ambaye amewahi kushikilia ubingwa wa Tanzania Light Heavyweight, ameongeza sura mpya kwenye wasifu wake kwa kufanikiwa kubeba mkanda wa IBO, mmoja wa mikanda inayotambuliwa kimataifa na kuchukuliwa kama ngazi ya kuelekea ubingwa wa dunia katika ngumi za kulipwa.
Ushindi huo ni hatua kubwa kwa ngumi za kulipwa nchini, na miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi kuwahi kupatikana na mabondia wa Kitanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Mashabiki na wadau wa mchezo huo tayari wameanza kuutaja ushindi wa Shoti kama “historia mpya ya ngumi za Tanzania”, wakimtaka Mtanzania huyo kuungwa mkono zaidi ili afungue milango kwa mabondia wengine wa ndani kufika kwenye viwango hivyo.
Baada ya kutwaa taji hilo la IBO International Middleweight, matarajio sasa ni kuona kama Shoti atapata nafasi zaidi za mapambano makubwa barani Ulaya na duniani, na kama ushindi huu utageuzwa kuwa msingi wa safari ya kuelekea mikanda mikubwa ya dunia katika uzito wa middleweight.
#Familiamoja #AhsantekwaTime