Wenyeviti wa Mitaa yote 27 kutoka katika kata za Njombe Mijini, Ramadhani na Mjimwema wamefanya ziara ya kutembelea miradi ya NJUWASA inayokwenda kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira katika Mji wa Njombe pamoja na chanzo cha maji Ijunilo.
Ziara hiyo imeongozwa na Mkurugenzi mtendaji Mha. Robert Lupoja ambapo Wenyeviti hao wametembelea jumla ya miradi mitatu inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa maji Lugenge, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya majitaka - Ngalanga na mradi mkubwa wa Miji 28 Njombe pamoja na chanzo cha maji Ijunilo.
Katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji aliwaomba Wenyeviti hao kushirikiana na NJUWASA katika utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kutoa elimu kwa Wananchi kutokana na athari kubwa iliyojitokeza ya kupungua kwa kiwango cha uzalishaji maji kwenye vyanzo vya vya maji vya Mamlaka hasa chanzo cha maji Ijunilo kulikosababishwa na shughuli za kibinadamu hasa kilimo zinazoendelea kufanyika kwenye maeneo ya vyanzo.
Aidha, Mkurugenzi alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma za maji kupitia miradi inayoendelea kutekelezwa mojawapo ya miradi hiyo ni mradi wa maji Lugenge ambao unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi huu na kuongeza kiasi Cha maji lita milioni 1.2 kwa siku, na mradi mkubwa wa maji wa miji 28 Njombe ambao utamalizika may- 2026 ambao utaongeza lita milioni 11 kwa siku.
Katika kuhitimisha ziara hiyo Mkurugenzi mtendaji Mha. Robert Lupoja amewaomba Wenyeviti hao kuwa mabalozi wazuri kwa kutoa taarifa sahihi kwa Wananchi hasa kuhusu juhudi za Serikali zinazoendelea kwenye miradi hiyo katika kuhakikisha inaboresha huduma ya maji Njombe , sambamba na kuhimiza ushirikiano katika kutunza Mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha vyanzo hivyo vinakuwa endelevu.
Wenyeviti hao wameishukuru NJUWASA kwa ziara hiyo na fursa ya kutembelea miradi hiyo na wameipongeza Serikali kutokana na miradi hiyo inayokwenda kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye Mji wa Njombe.
#Familiamoja #AhsantekwaTime