Tanzania yajipanga kuzalisha bidhaa zitokanazo na madini nchini

Tanzania yaendelea kupiga hatua katika Mpango wa ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani madini kutokana na ujenzi wa kiwanda kipya cha usindikaji na uyeyushaji madini ya Nikeli na Shaba kufikia asilimia 85 ya ujenzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe.Rais .Dkt.Samia Suluhu Hassan yanayoelekeza kuwa shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje.

Hayo yameelezwa  Novemba 21 mwaka huu na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati anakagua kiwanda cha kusindika na kuyeyusha madini ya Nikeli na Shaba kilichopo eneo la Mayamaya , Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Mhe.Mavunde amesema kuwa, kiwanda kitawasha mtambo wake wa kwanza wa uzalishaji ifikapo mwezi Februari, 2026 ambapo mtambo huo utachakata tani 300 za mashapo kwa siku.

Akielezea kuhusu gharama za uwekezaji katika kiwanda hicho, Mhe. Mavunde amesema kuwa uwekezaji huu ni mkubwa utakapo kamilika utagharimu shilingi bilioni 37, hivyo amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kutumia fursa hiyo ya soko la uhakika kupeleka malighafi katika kiwanda. 

Aidha akifafanua kuhusu malengo ya kujenga viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani madini , Mhe.Mavunde amefafanua kuwa shabaha kubwa ni kuhakikisha Tanzania inakamilisha mnyororo wote wa thamani madini kuanzia uchimbaji mpaka uchakataji na uongezaji thamani ili kusafirisha nje ya nchi bidhaa zitokanazo na rasilimali madini badala kusafirisha madini ghafi kama ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Joachimu Nyingo amesema kuwa, anaipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka wawekezaji wa madini mkoani Dodoma, jambo linalopelekea kufikia viwanda 9 vya uongezaji thamani madini.

#Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii