MKAZI mmoja wa Nyamira ameelekea kortini kulenga kuzuia Mawaziri watatu kuendelea na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Nyamira katika eneo Kiabonyoru, kituo kilichoteuliwa na Rais William Ruto.
Bw Peter Ariga Mokaya, kupitia wakili Dorah Gogi, amewashtaki mawaziri Soipan Tuya (Defence), Bw Julius Ogamba (Elimu) na Bw William Kabogo wa Habari, Mawasilian na Uchumi wa Didijitali.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Tume ya Elimu ya Juu (CUE), Serikali ya Kaunti ya Nyamira, Chuo Kikuu cha Kisii na Mwanasheria Mkuu.
Hii ni kesi ya tatu inayopinga kujengwa kwa chuo kikuu cha Nyamira katika eneo la Kiabonyoru lililotambuliwa na Rais Ruto. Walalamishi wanadai eneo hilo sio bora ikilinganishwa na maeneo mengine yaliyopendekezwa na wakazi wa Nyamira.
Kesi ya hivi punde inajiri wiki chache baada ya Waziri Ogamba na mwenzake Bi Tuya kuongoza hafla ya kuweka jiwe la msingi kutoa nafasi ya ujenzi wa chuo hicho.
“Chuo hicho kilichopendekezwa kinatarajiwa kuwa bewa la Chuo Kikuu cha Kisii. Lakini hamna ushahidi unaoonyesha kuwa taratibu zilizowekwa Sheria ya Vyuo Vikuu Nambari 42 na Kanuni ya Vyuo Vikuu, 2014, zilifuatwa,” ikasema kesi hiyo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime