Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameelekeza Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuhakikisha wanamkamata na kuzuia hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha ukaguzi cha Pamoja kilichopo Muhalala mkoani Singida.
Dkt. Mwigulu amesema kuwa mkandarasi huyo aliaminiwa na Serikali kwa kupewa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati uliosimama kwa zaidi ya miaka nane tangu mwaka 2016. Mradi huo unaojengwa na kampuni ya Impresa di Costruzioni Ing. E. Mantovani S.p.A ulipaswa kukamilika mwaka 2018.
Ametoa agizo hilo leo Ijumaa tarehe 21 Novemba, 2025 wakati alipokagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida ambapo atakagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa jitihada zimefanyika za kuona mradi huo unaendelea lakini mkandarasi amekuwa akileta ugumu katika utekelezaji “Mkandarasi huyu alitangazwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi na alielekezwa ailipe fidia Tanzania kwasababu ameicheleweshea mradi”
“Naelekeza, Kamishna wa uhamiaji kamata hati yake ya kusafiria, asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe, hii ni hujuma ya waziwazi, hii ni dharau ya waziwazi anaifanyia nchi yetu, Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo, tumemuajiri, tunamlipa lakini anajiamulia Kama aendelee na kazi au asiendelee, huyu ni mhalifu akamatwe mpaka jambo hili liishe” amesisitiza Dkt. Mwigulu
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa wakandarasi wa nje wanapaswa kufahamu kuwa wanapokuja kufanya kazi hapa nchini, watambue Tanzania imewaajiri na wasijione kama wao ni mabosi.
“Ninaelekeza wale washirika wetu katika mradi huu, ndani ya mwezi huu jambo hili liwe limekwisha watuambie wanaendelea ama hawaendelei, na Kama hawataendelea Waziri wa Ujenzi uwapatie wakandarasi wadogo wamalizie kazi hii, hii nchi ni yetu na tunawajibu wa kuilinda, na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametuambia hatuna mjomba, tuna mama tu anaitwa Tanzania”
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Ujenzi ihakikishe inausimamia mradi huo ili ukamilike na itumie wakandarasi wazawa , “Ninawahakikishia mradi huu tutaujenga na kuukamilisha”
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amemuagiza Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdullah Ulega kuwaelekeza wakandarasi wote kuhakikisha kuwa kila aliyepewa kazi apime kama kazi aliyoifanya inaendana na thamani ya fedha alizopokea.
“Haya ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwamba kila mradi, thamani ya fedha iendane na kazi ambayo imeshafanyika, sisi wasaidizi wake tutafuatilia maelekezo haya, hatuwezi ruhusu watu wachezee nchi yetu”
Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania kuilinda Tanzania, ili iendelee kuwa na maendeleo “Mungu ametupa nchi nzuri, nchi hii si mali ya viongozi, nchi hii sio mali ya vyama vya siasa, nchi hii ni yetu sote”
Kwa Upande wake, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema kuwa mradi huo ni mradi wa kielelezo na unafaida nyingi sana ambazo zitalisaidia Taifa ikiwemo kuokoa fedha nyingi zinazowekwa kwenye barabara.
“Vilevile eneo hili litakuwa ni eneo la kibiashara kwasababu watu watapata nafasi ya kufanya biashara na wananchi kutengeneza uchumi wao, sisi Wizara ya ujenzi tupo tayari kujenga ili mradi hui urejee” amesisitiza Waziri Ulega
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime