Nchini Cameroon, kiongozi wa upinzani Issa Tchiroma Bakary ametangaza siku nyingine ya watu "kusalia numbani" leo Ijumaa, Novemba 21, kwa heshima, aliyoitaja, kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi. "Ofisi za setikali na sekta binafsi, shule, shughuli za kiuchumi, kila kitu lazima kifungwe nchini kote," ametangaza katika wito wake.
Mgombea huyo, aliyetangazwa wa pili katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 12 na ambaye anajiona mshindi halali, kwa hivyo anajaribu kuweka shinikizo kwa serikali.
Katika video iliyotolewa siku ya Alhamisi, Novemba 20, kiongozi wa upinzani Issa Tchiroma Bakary, mgombea katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 12 nchini Cameroon, ametangaza kwamba "wale waliouawa kwa risasi za vikosi vya usalama ni mashujaa." Kiongozi huyo wa upinzani aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais, kulingana na matokeo rasmi ya Baraza la Katiba, anaainisha kwamba watu 48 waliuawa na vikosi vya usalama walipokuwa wakishiriki maandamano ya amani. Idadi hii bado haijathibitishwa na viongozi serikalini, ambapo makadirio yake ya hivi karibuni yalikuwa ya vifo 16.
Siku ya watu "kusalia nyumbani" leoIjumaa hii, Novemba 21 anayoitetea, ni, anasema, "katika moyo wa kutafakari, upinzani wa raia, na kwa maslahi ya pamoja ya taifa." Kauli hii inakuja karibu wiki mbili baada ya saa 48 alizotoa kwa serikali ya Yaoundé. Wakati huo, alidai kuachiliwa kwa wale wote waliokamatwa wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi.
Serikali ilikuwa imekiri kuachiliwa kwa takriban watu sitini, lakini kwa Issa Tchiroma, hii si kweli, na maelfu ya watu bado wako kizuizini, huku watu wengine kadhaa wameendelea kukamatwa. Mahali ambapo video hiyo ilitolewa haijabainishwa, lakini kulingana na vyanzo vilivyo karibu naye, Issa Tchiroma Bakary sasa yuko salama katika nchi ya kigeni.
Kutoka eneo hili ambalo halijafichuliwa kwa sasa, anadai anaweza kuunda na kupanga upinzani dhidi ya utawala wa Yaoundé. Kitendo kimoja cha upinzani kama hicho kilikuwa uteuzi wa wakili Alice Nkom siku chache zilizopita kama msemaji wake rasmi, akitumia barua yenye muhuri wa nchi na nembo, yenye maandishi chini "Rais-Mteule".