Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na viongozi wa majimbo 16 wametangaza mipango ya kuondoa vizuizi vya kukabiliana na Covid-19 kufikia mwishoni mwa mwezi Machi. Mipango hiyo itashuhudia vizuizi vingi vikiondolewa taratibu katika kipindi cha awamu tatu. Uamuzi huo unafuatia tangazo la waziri wa afya wa Ujerumani Karl Lauterbach aliyesema wimbi la kirusi cha Omicron tayari limefikia kilele. Maambukizi ya kila siku yameanza kupungua.
Kansela Scholz amesisitiza kuwa pamoja na kuwepo matumaini, janga la Covid-19 bado halijaisha. Sharti la watu kuvaa barakoa katika vyombo vya usafiri wa umma litaendelea kutumika pamoja na upimaji katika baadhi ya maeneo. Wabunge wa Ujerumani wamekuwa wakijadili hoja ya kuanzisha chanjo ya lazima ya Covid-19. Hii ni kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya watu ambao bado wanakataa kuchanjwa.