Washtakiwa 93 waliokamatwa kwa kesi za uharibifu wa mali, kufanya Vurugu na unyang'anyi wa kutumia silaha Novemba 19 walifikishwa tena katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza huku upande wa Jamhuri ukitakiwa kukamilisha ushahidi haraka katika kosa la kwanza la uharibifu wa mali.
Katika Shauri hilo la jinai namba 26546 la mwaka huu, washtakiwa hao 93 wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 326 (1) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023 kwa kosa la kwanza na kifungu cha 287 A cha Sheria hiyo.
Washtakiwa hao ni kati ya 172 waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka mbalimbali Wilayani Nyamagana kufuatia matukio ya vurugu yaliyotokea kati ya Oktoba 29 na 31, mwaka huu.
Shauri hili limetajwa kwa mara ya pili Novemba 19 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Amani Sumari baada ya kutajwa kwa mara ya kwanza Novemba 7, mwaka huu.
Kesi hiyo iliambatana na umati wa watu nje ya viunga vya mahakama hiyo, wakitarajia kuona ndugu zao wakiachiwa, wakiongozwa na agizo la hivi karibuni la Rais Samia Suluhu Hassan la kuvitaka vyombo vya dola kuchuja washtakiwa hao na kuwaachia wale waliofuata mkumbo.
Katika Mahakama, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Tunu Msangi na Prince Masawe, huku utetezi ukiwakilishwa na Mawakili kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Duttu Chebwa na Beatus Linda.
Mwanzo wa shauri hili, Wakili wa Serikali, Tunu Msangi, aliwasilisha ombi la kubadilisha hati ya mashtaka ili kuongeza washtakiwa wengine sita (6) ambao hawakuwa wamejumuishwa hapo awali.
Pia aliomba muda wa siku 90 wa kufanya upelelezi zaidi, akisisitiza kuwa upelelezi wa mashtaka yote mawili bado haujakamilika.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Duttu Chebwa, ulipinga vikali hoja ya kuongeza muda wa upelelezi, ukihoji kwa nini upelelezi unachukua muda mrefu katika kosa la kwanza la kuharibu mali. Chebwa alisisitiza kuwa hati ya mashtaka inaeleza wazi mali zilizoharibiwa na maeneo husika na hivyo wanashangazwa ni maelezo gani zaidi yanahitajika kukamilisha ushahidi.
#Familiamoja #AhsantekwaTime