Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Ofisi hiyo imepanga kupanua wigo wa elimu ya Muungano na Mazingira kwa wadau ikiwemo vyombo vya habari.
Amesema hayo wakati wa mazungumzo yake na Viongozi na Menejimenti ya Ofisi hiyo muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan, Dodoma Novemba 18, 2025.
Masauni amesema iwapo vyombo vya habari vina nafasi kubwa yenye umuhimu wa kipekee katika kuelimisha, kujenga na kuimarisha mshikamano katika jamii.
"Tutakaa pamoja na wahariri wa vyombo vya habari ili kushauriana na kuweka mikakati ya pamoja katika utoaji wa elimu ya Muungano na Mazingira" amesema Masauni.
Amesisitiza kuwa utoaji elimu kuhusu Muungano utagusa makundi yote ya kijamii hususani vijana na watoto hatua inayolenga kuimarisha msingi na faida za Muungano.
Aidha Masauni amesisitiza wito wa kutolewa kwa elimu hiyo ili jamii iweze kufahamu umuhimu wa Muungano, historia yake pamoja na faida zake.
Kuhusu Mazingira, Masauni amesema Serikali imepanga kutumia mbinu na njia mbalimbali za utafutaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"Suala la mazingira limejikita zaidi katika uhifadhi na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, lakini pia ni sekta mpya ya kiuchumi yenye uwezo wa kuzalisha mapato, ajira, na kukuza pato la taifa" amesema Mhandisi Masauni.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mbali na Muungano na Mazingira pia Uchumi wa Buluu nao utapewa kipau mbele sababu ni eneo ambalo likisimamiwa vizuri litasaidia kuongeza pata la taifa.
Amesema elimu ikitolewa vizuri na jamii ikaelewa kuhusu Uchumi wa Buluu itasaidia vijana kupata ajira na kuongeza vipato kwa wananchi na mwisho wa siku kila mmoja anakuwa na wajibu katika Utunzaji na Uhifadhi wa mazingira.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime