Vyombo vya habari vya serikali ya Syria vimeripoti kuwa Israel imeushambulia kwa makombora mji wa kusini mwa Damascus jana jioni, na kusababisha uharibifu wa mali. Hilo ni shambulio la pili la anga kufanywa na Israel dhidi ya Syria ndani ya mwezi huu. Shambulio jingine lilifanyika Februari 9 na kuzilenga betri za kutungulia ndege, katika hatua ya ulipaji kisasi dhidi ya kombora lililorushwa kutokea Syria. Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Syria, Rami Abdel Rahman amesema mashambulizi hayo yamekilenga kituo cha kijeshi cha serikali. Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka nchini Syria mwaka 2011, Israel imefanya mamia ya mashambulizi ya angani, yakilenga maeneo ya serikali pamoja na vikosi vinavyoungwa mkono na Iran na wapiganaji wa vuguvugu la wanamgambo wa Kishia la Hezbollah.