Arsenal kumaliza mkataba wake wa udhamini na Rwanda msimu ujao

Klabu ya soka ya Uingereza, Arsenal imetangaza kuwa itamaliza mkataba wake wa udhamini wa miaka nane na Visit Rwanda mwishoni mwa msimu wa 2025-26, ushirikiano uliokuwa kuwa na thamani yad ola milioni 13 kwa mwaka.

Mkataba huu wa udhamini kati ya klabu hiyo na Bodi ya utalii ya Rwanda, ulikosolewa tangu awali kutokana na kile kimetajwa kuwa kuhusika kwa nchi ya Rwanda katika mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kupitia tovuti yake, Arsenal imesema mkataba huo umeisha kwa makubaliano ya pande zote na kwamba umevuka malengo yake ya awali, alinukuliwa afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Richard Garlick.

Hata hivyo nembo ya Visit Rwanda bado itaendelea kuonekana barani Ulaya ambapo mwezi April mwaka huu bodi ya utalii ya Rwanda iliongeza mkataba wake na klabu ya Ufaransa, PSG hadi mwaka 2028, huku klabu ya Atletico Madrid ya Uhispania na yenyewe ikiingia mkataba wa miaka 3 kwa nembo hiyo kuonekana katika sehemu ya mkono ya jezi zake.

Mwezi Februari, serikali ya DRC ilitoa wito kwa klabu za Arsenal, PSG na Beyern Munich kusitisha mikataba na Rwanda kutokana na uhusika wake kwenye mzozo wa mashariki mwa nchi.

Aidha mwezi Septemba Rwanda ilipeleka soko lake la utalii nchini Marekani, ambapo ilitiliana Saini mikataba ya ufadhili na vilabu vya mpira vya ligi ya NFL Los Angeles Rams na ile ya mpira wa kikapu Los Angeles Clippers.

Uamuzi wa klabu ya Arsenal, umepokelewa kwa heshima na wanaharakati wa masuala ya amabi ambao wanasema hata hivyo umekuja kwa kuchelewa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii