Mtwara wakazi 150 wakabidhiwa hati miliki za ardhi

Zaidi ya wakazi 150 wa Mtaa wa Mbae Mashariki, Kata ya Ufukoni, Manispaa ya Mtwara-Mikindani wamepokea hati miliki za maeneo yao kupitia Kliniki ya Ardhi inayoendeshwa Kata kwa Kata.

Kliniki hiyo maalum inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Halmashauri ya Manispaa hiyo ambayo ilianza rasmi Novemba 17 mwaka huu katika Ofisi ya mtaa huo.

Wananchi walipokea huduma hiyo kupitia Kliniki ya Ardhi na kutoa pongezi kwa Serikali kwa kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.

Huduma hiyo imewavutia wananchi kutokana na huduma mbalimbali za ardhi zinazotolewa ikiwemo upatikanaji wa hati miliki, usajili kupitia mfumo wa e-Ardhi, elimu ya ardhi, uhamisho wa miliki pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Bw. Rugembe Maiga, amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa ambao ni ushahidi kuwa wananchi wanathamini umiliki halali wa ardhi pamoja na wanahitaji huduma rafiki, za haraka na karibu yao.

Mmoja wa wanufaika, Bw. Richard Evans, mkazi wa Ufukoni, amepongeza juhudi hizo za Serikali akisema: ''Naishukuru Serikali kwa kutumilikisha ardhi na kutupatia hati. Hati ni kinga na heshima kwa mmiliki, inakufanya utambulike kisheria na inalinda maslahi yako dhidi ya uvamizi au uhitaji wa kitaifa.”

Kliniki hiyo itaendelea hadi Novemba 23 mwaka huu na inatarajiwa kufanyika pia katika Kata ya Likombe kuanzia Novemba 24 - 30 mwaka huu ikilenga wananchi wote kupata haki ya kumiliki ardhi kihalali na kwa utaratibu sahihi.

#Familiamoja

#AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii