Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM TAMISEMI) akisisitiza kuwa dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.
Akizungumza Jijini Dodoma wakati wa kumkabidhi ofisi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe Mhe. Mchengerwa alimesema wizara hizo mbili zimeunganishwa na majukumu yao hususani katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
“Wizara ya Afya na TAMISEMI ni wizara zilizoshikamana. Nikuahidi Mhe. Waziri kuwa tutahakikisha hakuna mkwamo katika utekelezaji wa majukumu ya afya. Dhamira yetu ni kuwahudumia wananchi na kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza malengo yake ya kuleta maendeleo,” amesema Mchengerwa.
Ameongeza kuwa Sekta ya Afya haiwezi kutenganishwa na TAMISEMI, kwani utekelezaji wa huduma nyingi za afya unawafikia wananchi kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Lengo letu ni kuhakikisha Mtanzania anapata huduma bora, kwa wakati, na katika mazingira rafiki. Tunataka kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao,” amesisitiza
Katika hatua nyingine, Mchengerwa aliwashukuru watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake, akiwapongeza kwa bidii na mshikamano uliosaidia kufanikisha malengo mbalimbali ya serikali.
“Hapa kuna timu nzuri sana. Watumishi hawa wana uwezo wa kusukuma ajenda za Mheshimiwa Rais, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kufanikisha malengo yaliyowekwa. Ninaamini timu hii itakuongoza vizuri katika utendaji,” amesema Mchengerwa
Kwa upande wake, Mhe.Prof. Shemdoe alimshukuru Waziri Mchengerwa kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuahidi kuendeleza jitihada za kuinua huduma za afya katika ngazi za Serikali za Mitaa.
Hata hivyo Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wizara na taasisi zake katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo na Ilani ya Chama Tawala.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime