Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amewataka Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kutambua kwamba maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Hassan kuhusu kutumia fedha za ndani zinazotokana na rasilimali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ni agizo linaloigusa Wizara ya Madini moja kwa moja.
Ameyasema hayo Novemba 18 mwaka huu wakati akizungumza na Watumishi wa Wizara ya madini na taasisi zake Makao Makuu ya Wizara Mtumba, mapema baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino Dodoma na Rais Dkt. Samia Hassan.
Mhe. Mavunde ameeleza kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa na imani kubwa na Wizara ya Madini hususan kutokana na mapato yanayotokana na rasilimali madini kuendesha uchumi wa nchi na hivyo kumtaka kila mtumishi kutumia nafasi yake kuhakikisha sekta ya madini inagusa maisha ya kila mwananchi kwa manufaa ya jamii na taifa.
Aidha akielezea kuhusu programu ya Mining for A Brighter Tomorrow (MBT), Mhe. Mavunde amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kikamilifu kama ulivyopangwa kwa lengo la kuwawezesha wachimbaji vijana na wanawake kuchimba kwa tija.
Kupitia mradi wa MBT Wizara imepanga kuwawezesha vijana na wanawake kwa kuwapatia maeneo ya kuchimba na teknolojia ili kuwarahisishia shughuli zao.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kumshukuru Dkt. Samia kwa kumuamini na kumrejesha tena kuitumika wizara hiyo pamoja na kuwashukuru watumishi wote na wadau wote wa Sekta ya madini kwa ushirikiano mkubwa.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime