Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume Huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka imesema Rais ameunda tume hiyo kutokana na mamlaka aliyo nayo chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, na inalenga kutoa uchambuzi wa kina wa matukio hayo, pamoja na kupendekeza hatua za kisheria na za kitaifa ili kuhakikisha amani na usalama unadumishwa katika Taifa.
Rais amemteua Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mohamed Chande Othman kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wajumbe walioteuliwa ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue, Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu Balozi Radhia Msuya.
Wajumbe wengine katika Tume hiyo ni Balozi Lt. Gen. Paul Meela (Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu), Said Mwema (Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Mstaafu), Balozi David Каруа (Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu), na Dkt.
Stergomena Lawrence Tax (Aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC).
Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi imesema kuwa Tume hiyo itafanya kazi kwa uwazi na kwa haraka, huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau wote wa serikali na jamii ili kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa ufanisi.