Mwili wa Mtanzania Joshua Mollel waagwa nchini Israel

Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilifanya ibada ya kuuaga mwili wa Mtanzania Joshua Loitu  Novemba  18 mwqka huu katika Mnara wa Mashujaa, uliopo Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mhe. Sharen Haskel, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Wanadiplomasia, Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Watanzania waishio Israel, Waisrael walioguswa na msiba huu na Wanahabari.

Hafla hiyo pia ilirushwa mubashara kutoa fursa kwa wanafamilia na walioguswa na msiba huu kufuatilia tukio hilo.

Katika hotuba yake, Mhe. Balozi Kallua alitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mzee Mollel na Tanzania kwa ujumla kwa kumpoteza kijana Joshua, ambaye alikuwa na ndoto kubwa ya kujishughulisha na kilimo biashara baada ya kumaliza mafunzo yake.

Aidha, Balozi Kallua alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Israel, Jeshi la Israel na wale wote waliopambana bila kuchoka kuhakikisha kuwa mwili wa Joshua na miili ya wahanga wengine wa tukio hilo inarejeshwa nchini Israel.

Vilevile, aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Israel katika kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.

Hivyo naibu Waziri Haskel alitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mzee Mollel kwa kumpoteza kijana wao, ambaye alikatizwa uhai wake kinyama na kundi la Hamas.

Aidha alisikitika kusema kuwa Israel haikuweza kuulinda uhai wa Joshua pamoja na Waisrael wengine zaidi ya 1000 waliopoteza maisha kutokana na uvamizi huo.

Vilevile alisema kuwa Israel ilitoa umuhimu katika kuhakikisha kuwa mwili wa Joshua unapatikana kama ambavyo ilifanya kwa raia wake, na kwamba ilibidi kubadilishana na wafungwa ili mradi kufanikisha suala hilo.

Kwa upande wake naibu Waziri Haskel alitumia fursa hiyo kuahidi kuwa Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha zaidi mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili. 

Hata hivyo katika hotuba zingine zilizotolewa katika hafla hiyo ni pamoja na ya Mkurugenzi wa MASHAV; Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Dawati la Wageni.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii