Jurgen Klopp atoa sababu za kukataa kuifundisha Manchester United

Aliyekuwa kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp, amefichua sababu zilizomfanya kukataa ofa ya kujiunga na Manchester United kabla ya kuchukua mikoba ya Liverpool mwaka 2015.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Klopp alisema hakuvutiwa na mpangilio na maono ya muda mrefu ya United wakati huo, akieleza kuwa hakuhisi uwepo wa dira thabiti ya maendeleo ndani ya klabu hiyo.

“Nilihisi Liverpool wana uelekeo sahihi na dhamira ya kweli ya kujenga kitu cha kudumu. Sikuwa na hisia hizo kwa United wakati huo,” alisema Klopp.

Kocha huyo raia wa Ujerumani alijiunga na Liverpool Oktoba 2015 akitokea Borussia Dortmund, na tangu wakati huo aliibadilisha klabu hiyo kuwa moja ya timu zenye mafanikio makubwa barani Ulaya.

Chini ya Klopp, Liverpool ilitwaa mataji kadhaa makubwa ikiwemo Ligi Kuu ya England (Premier League) msimu wa 2019/2020 na Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) mwaka 2019, pamoja na Kombe la Dunia la Klabu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii